Friday, August 26, 2016



Waebrania 10:19-20
"Basi ndugu, kwa kuwa tuna ujasiri wa kupaingia patakatifu kwa damu ya Yesu, njia ile aliyotuanzia iliyo mpya, iliyohai, ipitayo katika pazia, yaani mwili wake."

Kuingia patakatifu ni kuingia chumba cha enzi ya Mungu, tukumbuke kuwa Mungu ni Mungu mwenye enzi, Mtawala wa Mbinguni na Duniani.  Mtu anayeingia mahali patakatifu anapaswa awe na ujasiri wa kusimama mbele ya Mungu.  Ujasiri huo tunaupata katika damu ya Yesu Kristo ambayo ndiyo inayotutakasa na uovu wetu wote

1 Yoh 1:7
"Bali tukienenda nuruni, kama yeye alivyo katika nuru, twashirikiana sisi kwa sisi, na damu yake Yesu, yatusafisha dhambi yote,"

Tunajua ni muhimu kuwa safi kabla ya kuingia mahali patakatifu pa Mungu kama Taifa la Israeli lilivyokuwa likifanya hekaluni.  Na sasa katika Yesu Kristo ambaye bdiye kuhani wetu mkuu, yeye anatuongoza katika kuingia mahali patakatifu pasipotengenezwa na binadamu ila Mungu mwenyewe tukiwa safi na ujasiri wake.

Ipo njia ya mtu kupita na kuishi ili aweze kuingia mahali patakatifu, njia mpya na ni hai, hiyo njia ndiyo ipitayo katika pazia la mahali patakatifu na njia hiyo ni mwili wake Yesu Kristo.  Tukumbuke Kristo alisema kuwa yeye ni njia, na ukweli, na uzima, na hakuna afikaye kwa BABA (MUNGU) ila kupitia kwake tu.

Yohana 14:6
"Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi."

Hivyo ni vema kumjua Yesu Kristo ili tuweze kumjua Mungu, pia tumfikie Kristo na kuishi ndani ya Kristo ili tuweze kumfikia Mungu na kuishi ndani ya Mungu.  Katika Mwili wa Yesu Kristo, kanisa, ushirika na Roho wa Mungu, tunaimarika ili tuweze kupita katika pazia la mahali patakatifu na kuweza kusimama mbele yake Mungu kama Baba yetu na siyo Mhukumu wetu wetu.

Upendo wa Mungu kwetu ni MKUBWA SANA, na ndani ya Yesu Kristo Pendo la Mungu limekamilika daima na milele.  Mungu hapendi watu wake wawe mbali naye, aidha watu hao ni wakristo au bado hawajaamini ndani ya Neno la Mungu, Habari njema kwa ulimwengu wote.

Mungu ametupatia Mwana wake wa pekee Yesu Kristo ili tuokolewe kwake, tudumu katika pendo lake na kuishi katika umoja naye.

Ewe binadamu, chukua muda hu kusali sala hii fupi hata kimoyomoyo kama upo katika mazingira au ugumu wa kutoweza kuisema kwa sauti ya kinywa chako, kwa maana Mungu anasikia hata yale ya Moyoni mwa Mtu.  Na Mungu ambaye ni mwaminifu atakusamehe ya kuyafungua maisha yako katika safari mpya ya kuishi pamoja na Kristo, na katika mwili wa Kristo.

Hata kama wewe ni Mchawi au Jambazi au umetenda uovu mwingi mpaka una mashaka ya kuongea mbele za Mungu, Kristo Yesu alikuja duniani na mpaka leo yupo na Mungu ili uwe huru, Yesu Kristo wagonjwa wanaoelemewa na dhambi  na uovu wa Dunia hii na Shetani mwovu wapate kupona kwa kupokea tiba ya wokovu wake na kufanyika viumbe wapya, wawe na ufufuo wa Mungu na uzima wa milele wawe nao tele.


SALI SALA HII

Mwenyezi Mungu naomba unisikie,
na kwa huruma zako nyingi nifadhili Roho yangu.
Naungama kwako uovu wangu, nakuomba unioshe
kwa Damu ya Yesu Kristo,
yeye ambaye ni Kweli, ni njia, na Uzima.
Yesu naomba unipokee niishi upya ndani yako,
na katika ufalme wako Mbinguni.
Nidumishe nawe ili niweze kuingia mahali pako 
PATAKATIFU.
Niponye mauti ya dhambi zangu, niwekee uzima wako
wa milele ndani yangu.
Nakuomba kwa Jina lako Takatifu
YESU KRISTO.

AMINA.


Shirikisha fundisho hili na sala hii pia kwa wengine,
na Mungu akubariki na kukutegemeza daima katika Yesu Kristo.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Powered by Blogger.

Popular Posts